Jumapili , 1st Mei , 2016

Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuwaendeleza kielimu watoto wao walioishia elimu msingi ili waweze kunufaika na uwekezaji unaofanyika kupitia kampuni mbalimbali.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally

Akizungumza katika mahafali ya kuhitimu mafunzo ya hoteli yaliyofanyika katika Hoteli ya Old Boma, Mikindani, Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, amesema vijana wengi wanahangaika kutafuta ajira kutokana na kukosa elimu kwa sababu wengi wao wana elimu ya msingi ambayo haiwezi kuwapatia ajira itakayokidhi mahitaji yao.

Aidha, amelipongeza shirika la Trade Aid ambalo ndio wanaondesha mafunzo hayo kwa wahitimu katika Hoteli hiyo ya kitalii iliyopo katika mji wa Mikindani, kwa kushirikiana na wakazi wa mji huo na kuweza kuendeleza miradi mbalimbali ikiwamo kuendesha hoteli hiyo.

Naye, Meneja Mradi wa Shirika hilo Bw. Emmanuel Mwambe, amesema shirika lilianza ukarabati wa jengo la Old Boma mwaka 1999 ambapo lilipata kibali kutoka katika serikali ya wilaya na miaka mitano baadaye ikafunguliwa hoteli kwa malengo ya kuisaidia jamii ya wakazi wa Mikindani na Mtwara kwa ujumla.

Amina Mussa, ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa mafunzo hayo, amesema amefurahishwa na hatua ya kuhitimu kwani baada ya hapo anatarajia kupata ajira kupitia ujuzi wa masuala ya hoteli ambao ameupata katika kipindi chote cha mafunzo, huku akiwataka vijana wengine kuchangamkia kujiunga na mafunzo hayo yanayotolewa bila malipo.