Jumatatu , 10th Oct , 2022

Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwamo vya ubakaji na ulawiti, wazazi na walezi wametakiwa kupunguza ukali kwa watoto na kujenga mazoea ya kuzungumza nao kama marafiki, ili kupunguza vitendo hivyo kwa kundi hilo

Wakizungumza wakati wa sherehe za Michael na Watoto, baadhi ya waumini wa kanisa la Anglikana dayosisi ya Lweru wamesema kuwa wazazi na walezi wanapozidisha ukali kwa watoto na kushindwa kutenga muda wa kuzungumza nao ili kusikiliza changamoto zinazowakabili, wanasababisha kuwa mbali nao, na kuwaweka katika mazingira hatarishi ya kufanyiwa ukatili.

"Sisi wazazi ambao tunalea watoto, pale unapojifanya kuwa bize na mambo mengine, shetani pia anatumia muda huo kushughulika na watoto wako anachukua nafasi yako, ushauri wangu kwa wazazi inabidi tuwe karibu na watoto wetu zaidi ya tunavyokuwa karibu na vitu vingine ili tusiweze kuacha nafasi ya ulezi na uzazi mikononi mwa shetani" wamesema.

Kwa upande wake mchungaji Hosseah Baraseka ambaye ni mratibu wa Masomo ya Shule ya Jumapili pamoja na Vijana katika kanisa hilo, amesema kuwa kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa watoto kunatokana na jamii kuendekeza vitendo vya kishirikina.

"Wanajamii tumejisahau sana katika kulinda watoto dhidi ya ukatili, niombe kila mzazi au mlezi ajisikie kumsaidia mtoto ambaye unaona anafanyiwa vitendo hivyo, fikisheni taarifa mahali stahiki ukibaini kuna mtoto kafanyiwa ukatili." amesema