
Wazazi nchini wameombwa kutowafungia ndani watoto wenye ulemavu wa ngozi albino na badala yake wawapeleke shule pale wanapofikia umri wa kuanza shule ya awali.
Katibu wa Chama cha maalbino wilaya ya Temeke Bw. Gaston Mcheka amesema kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwafungia ndani watoto walemavu wa ngozi kwa kuona kuwa ni nuksi na mkosi katika familia zao.
Aidha Mcheka ameongeza kuwa wilaya hiyo imeanzisha mkakati maalum wa kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu wa ngozi wanapata elimu kwani ndiyo njia pekee ya kuwakomboa kwa kuzingatia kuwa ni jamii ambayo haiwezi kufanya kazi za kutumia nguvu au katika jua kutokana na ulemavu wa ngozi walio nao.
Hivyo amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza katika kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo vifaa vya kusomea,madaftari,lotion ya ngozi,kofia pana na miwani ya kusomea.
Mcheka ameongeza kuwa muda umefika, kwa jamii kuhakikisha wanaondokana na mawazo mgando ya kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu wa ngozi na kuwaona kuwa ni jamii moja kwani hali ya unyanyapaa inamsababishia albino kujiona kuwa ni kiumbe ambacho hakina thamani katika jamii.