Jumatano , 3rd Feb , 2016

Watu wawili wamefariki dunia Mkoani Mbeya huku mmoja akichinjwa na kutenganishwa kwa kiwiliwili na kichwa kisha kuchomwa moto na watu wasiofahamika kwa madai ya kuhusishwa na imani za kishirikina kwa kutuhumiwa kupeleka kipindupindu katika eneo lao

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi

Akithibitisha kutokea kwa matukio hayo kamanda wa polisi mkoa wa mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi amesema katika tukio la kwanza wazee wawili wakazi wa kitongoji cha Bulinda Wilaya ya Kyela mkoani mbeya waliuawa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao na kisha kuchomwa moto na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda Msangi aliwataja wazee hao waliouawa kuwa ni Geneli Kapwela [65] na Rahabu Bungulu [70] ambapo miili ya marehemu ilikutwa katika nyumba walimokuwa wakiishi mnamo tarehe 01.01.2016 majira ya saa 08:00 asubuhi huko kitongoji cha Bulinda, Kijiji/Kata ya Matema, tarafa ya Ntembela wilaya ya Kyela mkoa wa Mbeya.

Katika tukio hilo, Geneli Kapwela aliuawa kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili na kukatwa mkono wa kushoto na viungo hivyo hadi sasa havijulikani vilipo na Rahabu Bungulu aliuawa kwa kuchoma na kitu chenye ncha kali na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi.

Inadaiwa kuwa, wananchi hao walivamia nyumba waliyokuwa wakiishi marehemu hao kisha kuwakata na vitu vyenye ncha kali na baada ya kutekeleza mauaji hayo, watu hao waliangusha nyumba waliyokuwa wakiisha ambayo ilikuwa imejengwa kwa mianzi na kisha kuichoma moto.

Chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina kwani marehemu walikuwa wanatuhumiwa kuleta ugonjwa wa kipindupindu kijiji hapo kwa njia za kishirikina na watu wawili wamekamatwa kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo ambao ni Aliko Mwamtobe mkazi wa Matema na Alisolomon Mwamtobe [49] mkazi wa kitongoji cha Bulinda.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa jamii kuacha imani potofu za kishirikina kwani zina madhara makubwa katika jamii.