Kambi ya wagonjwa wa Kipindupindu wilayani Tarime
Watu wawili wamefariki dunia na wengine 39 wakilazwa katika kambi maalum ya ugonjwa wa kipindupindu katika kituo cha afya cha Nyamongo baada ya kuugua ugonjwa huo ambao umeibuka kwa mara ya kwanza katika mji huo wa Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara.
Kufuatia mlipuko huo mkubwa wa ugonjwa wa kipindipindu katika mji huo wa kibiashara wilayani Tarime, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, ikiongozwa na mwenyekiti wake bw Glorious Luoga, imelazimika kutumia zaidi ya saa sita kushiriki katika usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya mji huo, ikiwa ni njia moja wapo ya kukabiliana na ugonjwa huo unatokana na uchafu.
Nao baadhi ya viongozi na wananchi katika mji wa Nyamongo, wakizungumza wakati wakishiriki katika usafi huo wa mazingira, pamoja na kupongeza hatua ambayo imechukuliwa na kamati hiyo ya ulinzi na usalama kukubali kushirikiana na jamii katika zoezi hilo la usafi, wamesema hadi sasa watu kumi na wawili bado wamelazwa katika kituo hicho cha afya huku mwanamke mmoja akifariki dunia kwa ugonjwa huo na kuacha mtoto wa miezi mitatu
Tayari mkuu huyo wa wilaya ya Tarime ametoa siku saba kwa kila kaya katika eneo hilo kujenga vyoo na kwamba baada ya siku hizo kumalizika jeshi la polisi kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata wataendesha msako mkali wa nyumba hadi nyumba ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo .