Jumanne , 24th Mei , 2016

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage, amesema lengo la serikali hadi ifikapo mwaka 2020 ni kuhimiza wawekezaji kujenga viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage.

Akizungumza jana Bungeni mjini Dodoma, Waziri Mwijage amesema viwanda hivyo vitakavyotumia malighafi za ndani vitalenga sekta za kilimo na maliasili kwa kuzingatia fursa za jiografia na ambavyo vitatoa ajira na kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo.

Waziri Mwijage amesema kuwa sasa serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati nchini ili kutimiza lengo la kuwa na uchumi unaotegemea viwanda.

Aidha, Waziri huyo ameongeza kuwa uwekezaji huo utalenga kwenye ngazi za vijiji hadi mijini huku akisema mfaniko ya jukumu hilo yanahitaji ushirikiano kutoka ngazi ya kijiji hadi mkoa.

Ameongeza kuwa wizara yake kupitia kurugenzi ya viwanda na biashara ndogondogo pamoja na taasisi za SIDO,TANTRADE,TBS, na EPZA, zipo tayari kushirikian a na mamlaka ya mkoa wa Simiyu ili kuhamasisha ujenzi wa viwanda.