Jumatano , 16th Mar , 2016

Mamlaka ya Uendelezaji wa Maeneo Huru ya Uwekezaji EPZA imetakiwa kuhakikisha kuwa wawekezaji wanaopatiwa maeneo ya biashara na mamlaka hiyo wanatengeneza bidhaa kwa kutumia malighafi za hapa nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara Dkt Dalali Peter Kafumu.

Agizo hilo limetolewa tofauti na hali ilivyo sasa kwani wengi wa wafanyabiashara wanaopatiwa maeneo ya kujenga viwanda nchini wamekuwa wakiagiza malighafi wanazotumia katika viwanda vyao kutoka nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara Dkt Dalali Peter Kafumu, ametoa agizo hilo hii leo, muda mfupi baada ya kumaliza ziara ya kutembelea makao makuu ya EPZA ambapo kamati yake ilipata fursa ya kujionea viwanda vilivyojengwa katika eneo la EPZ la Benjamin Mkapa lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dkt Kafumu amesema ni Watanzania wachache wanaofahamu shughuli za mamlaka hiyo pamoja na fursa zilizopo kwenye Maeneo Huru ya Uwekezaji, ambapo ameutaka uongozi wa EPZA kuongeza elimu kwa umma ili wananchi pamoja na taasisi za umma, zichangamkie fursa hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.