Jumatano , 29th Aug , 2018

Mara nyingi kumekuwa na utata wa wana ndugu kugombea mali pindi mhusika anapofariki na jambo pekee linaloweza kumaliza hayo ni Wosia ambao unaachwa na marehemu, lakini katika kuandika inashauriwa kundi hili lisiwe sehemu ya mashahidi.

Kupitia kipindi cha MJADALA kinachoruka cha East Africa Television, Mwanasheria Suzan Charles kutoka Chama cha wanahabari wanawake nchini (TAMWA), ameeleza kuwa katika kuandika Wosia mhusika hatakiwi kumshirikisha mtu ambaye atarithi, kwasababu Wosia ni siri ya mwandishi mwenyewe na mashahidi ambao amewachagua.

Mwanasheria huyo amefafanua kuwa wosia unaweza kuandikwa na mtu yeyote ambaye ametimiza miaka 18, hata kama anamiliki simu ya mkononi tu anaweza kuandika na si lazima awe na mali nyingi kama ambavyo inafikirika. Pia amesema kuna aina mbili za wosia ambazo ni wosia wa tamko la mdomo pamoja na ule wa maandishi.

Katika wosia wa tamko la mdomo wanatakiwa kuwepo na mashahidi wanne ambao ni marafiki na ndugu mmoja au wawili. Kwa upande wa wosia wa maandishi wanatakiwa kuwepo mashahidi wawili ambao wanajua kusoma na kuandika na katika hao wawili lazima mmoja awe ndugu lakini asiwe miongoni mwa warithi wa mali iliyokusudiwa.

Inashauriwa kuwa wosia uhifadhiwe katika maeneo mbalimbali muhimu ambayo ni Mahakama au Wakala wa ufisilisi na udhamini (RITA) ama kwa mtu unayemwamini lakini asiwe miongoni mwa warithi. 

Sababu ya kutowahusisha warithi ni kuepusha migogoro miongoni mwa wahusika na pia inatoa nafasi kwa aliyeandika kuweza kubadilisha bila kuzua utata kwa wale ambao amewajumuisha kwenye urithi wake.