Jumanne , 14th Apr , 2015

WATU wanane wakiwemo wanafunzi sita wa darasa la kwanza katika shule ya msingi kibirizi Manispaa ya Kigoma ujiji wamekufa baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mjini kigoma kwa saa tatu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa kigoma Maweni,DK.FADHILI KIBAYA amesema sambamba na watu hao waliofariki pia watu 15 wamejeruhiwa katika tukio hilo

Dk.Kibaya amewataja waliofariki kuwa ni pamoja na Yusuf Athuman, Hassan Ally, Fatuma Sley, Zamda Seif, Shukrani Yohana na Warupe Kapupa ambao ni wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule hiyo ambapo Mwalim aliyefariki ametambuliwa kwa jina la Elieza Mbwambo aliyekuwa akifundisha darasa la tano.

Aidha pamoja na watu hao mtu mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Focas Ntahamba pia amefariki kwa kupigwa na radi katika eneo la Bangwe mjini kigoma.

Mmoja wa walimu wa shule ya msingi ya kibirizi,WILBERT EMANUEL ambaye alikuwepo eneo la tukio amesema kuwa wamesikitishwa na tukio hilo ambalo lilitokea bila kutegemea na kuacha simanzi kubwa shuleni hapo.

Hili ni tukio la pili kutokea mkoani kigoma ambapo takriban mwezi mmoja uliopita wanafunzi sita na mwalim wao walikufa baada ya kupigwa na radi katika shule ya msingi nyakasanda katika kijiji cha nyachenda wilayani kasulu .