Ijumaa , 26th Jun , 2015

Watoto wawili wenye umri wa kati ya miaka miwili na mitano wameuawa na fisi katika kijiji cha Mnkola kata ya Ibihwa Wilayani Bahi Mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti.

Mnyama aina ya Fisi ambae anasadikiwa kuwaua watoto wawili Mkoani Dodoma.

Akizungumza na East Africa Radio , mwenyekiti wa kitongoji cha Teya Kata ya Ilindi Wilayani Bahi, Paul Mwaja amesema kuwa watoto hao wameuawa katika matukio mawili ndani ya kipindi cha juma moja.

Amesema tukio la kwanza lilitokea juzi ambapo mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu aliuawa na fisi wakati akiwa wamelala na wenzie wawili.

Baba mzazi wa mtoto aliyeuawa usiku wa kuamkia leo aliyejitambulisha kwa jina la Mchamingi alisema kuwa hawana imani kama fisi huyo kuwa ni wa kawaida kwani katika tukio la kwanza kabla ya kuuawa alikimbilia katika kijiji cha jirani cha Bahi Makulu ambapo alipotelea kwenye nyumba za watu.

Amesema kuwa katika tukio la pili ambapo mwanaye aliuawa walilazimika kumfuatilia fisi huyo ambapo walimkuta amejificha kwenye mapango ya mawe ambapo hata hivyo walitumia risasi kumuua.

Alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea kijijini hapo kwani katika kipindi cha miaka yote iliyopita hakuna mtu aliyewahi kuuawa na fisi.