Ijumaa , 1st Jan , 2016

Mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi amesema kuwa atawaunganisha katika huduma za afya watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kuweza kutibiwa bure na kusema kuwa watoto hao huenda wanaugua mara kwa mara.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi

Dkt. Nchimbi Amesema kuwa watoto hao wataunganishwa katika mfuko wa afya ya jamii hii leo Januari Mosi Mwaka 2016 ambapo kutakuwa na chakula cha pamoja, huku akisema kuwa watoto hao wawe tayari kuitambua familia moja ambako watatunziwa kadi zao za matibabu na kutoa watakapohitaji tiba.

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu huyo wa mkoa ofisini kwake amesema kuwa watoto hao wanahitaji huduma ya afya na wakitibiwa wanaweza kuja kuwa watu wazuri hapo baadaye na kuwa wanaishi katika mazingira hayo sio kwa kupenda.

Amesema kuwa watoto hao huenda wanaugua mara nyingi zaidi kuliko kawaida lakini kupata kwao huduma huenda kukawa kikwazo kwao na kuishi maisha magumu kuliko kawaida.