
Watoto wenye ualbino
Ripoti hiyo imeonesha kuwa mikoa ambayo inaongoza kwa mauaji, ukatili na unyanyapaa dhidi ya walemavu wa ngozi nchini Tanzania imekuwa na kiwango kidogo cha matukio hayo katika kipindi cha miaka miwili baada ya kutolewa kwa elimu na watu kubadili mitizamo yao.
Ripoti hiyo imetolewa na shirika la UNESCO baada ya kutoa elimu katika wilaya nne ambazo zilikithiri kwa mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Simiyu.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo nchini Tanzania Bi. Zulmira Rodrigues amesema licha ya kubaini kuwepo na familia ambazo zinakatisha uhai wa watoto wachanga wanaozaliwa na ulemavu wa ngozi lakini wanafamilia, viongozi wa dini na waganga wa jadi wameonesha mwamko mkubwa wa kupinga ukatili dhidi ya watu wenye albinisim.
Abdallah Possi - Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Walemavu)
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Dkt. Abdallah Possi amesema, licha ya jamii ya Tanzania kuanza kutambua kuwa hakuna tofatu kati yao na watu wenye ulemavu wa ngozi, ni wakati sasa wa kushughulikia changamoto zingine zinazowakabili kama Elimu, Dawa na Mafuta ya kuwakinga dhidi ya mionzi ya jua.
Aidha, Nandera Ernest Mhando ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mtafiti mkuu amesema, hata wanganga wa jadi wameanza kutoa taarifa wanapoletewa viungo vya watu wenye ulemavu.