Ijumaa , 12th Feb , 2016

Serikali imewasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.

Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Februari 12, 2016 ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.

“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika, pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi, ambaye ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.

Pia Waziri Mkuu amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi, ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika, hatua rasmi zitachukuliwa na iwapo itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.

Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika, na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.

Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni, amabazo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).