Ijumaa , 6th Mar , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Subilaga Kapange, pamoja na maafisa wengine wawili wanaosimamia ukusanyaji wa mapato katika kituo cha mabasi cha Korogwe, baada ya kushindwa kuwasilisha mapato Serikalini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ameyasema hayo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Tanga, huku wengine ambao amewasimamisha kazi ni Meneja wa Kituo cha mabasi Majid Salehe na msaidizi wake.

"Mnakusanya fedha na kuziweka mfukoni, hazipelekwi benki mnazitumia kwa matumizi yenu binafsi na kuna siku inaonesha hamjakusanya chochote, hatuwezi kuvumia hali hii, hawa wote wakamatwe na wawekwe ndani na hii iwe funzo kwa waweka hazina wote nchini" amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema kuwa Halmashauri hiyo ya Mji Korogwe, imejenga kituo cha mabasi lakini makusanyo yake hayafikishwi Serikalini, huku baadhi ya wazabuni waliopewa kazi hiyo wakiwa hawana hata mikataba, jambo linalochangia Halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji.