Kamanda wa Polisi Mkoani humo ACP-Henry Mwaibambe
Akizungumza leo na waandishi wa habari, kamanda wa polisi mkoani humo ACP-Henry Mwaibambe, amesema katika upekuzi walioufanya juzi usiku nyumbani kwa Musa Kais, walifanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya kutengenezea milipuko ikiwa ni pamoja na viwashio (Fuse) 44, Detonator 39, Explogel-Nusu kipande na fedha kiasi cha sh. 353,000.
Aidha, alisema watuhumiwa wengine katika nyakati tofauti, walikamatwa na malighafi za kutengenezea milipuko hiyo ambayo ni, Mbolea Kg 6, Kg tatu zikiwa zimechanganywa na Explogel, chupa sita za milipuko ambazo zilikuwa tayari zimechanganywa kwa ajili ya kulipuliwa, waya wa vilipuzi wenye urefu wa mita tano na nusu na vipande vingine, pamoja na majongoo ya Bahari 55.
Amesema, ni wajibu kwa wananchi wa Mtwara kushirikiana na jeshi la polisi kuweza kuutambua mtandao huo na kuwakamata, na kwamba watuhumiwa hao wanahojiwa na baada ya muda mfupi watafikishwa mahakamani.