Watu watatu wamefariki dunia, wawili papo hapo na wengine 35 kujeruhiwa, kati yao wanne vibaya baàda ya basi walilokuwa wakisafiria kutokea jijini Dar es salaam kuelekea Morogoro, mali ya kampuni ya BM kuligonga ubavuni lori lililokuwa likija mbele yake na kuangukia kwenye bonde pembeni ya barabara na kupinduka mara nne, katika eneo la Lubungo Mikese,barabara kuu ya Morogoro- Dar es salaam.
EATV imefika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro na kushudia majeruhi wa basi hilo wakiletwa kwa magari binafsi na basi lingine la kampuni hiyo,wakionekana kujeruhiwa zaidi maeneo ya kichwani,usoni na miguuni.
Mwandishi wa habari hii alilazimika kuweka kalamu pembeni na kusaidiana na wananchi wengine kuwabeba majeruhi na kuwaingiza kwa madaktari kupata huduma ya kwanza, huku vitanda vya kuwabebea vikionekana kuwa vichache ikilinganishwa na wingi wa majeruhi.
Baadhi ya majeruhi waliohojiwa wameeleza namna ajali hiyo ilivyotokea na kulalamikia wizi uliofanywa na watu waliofika eneo la tukio baada ya ajali...
Daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, Francis Semwene amekiri kupokea miili ya wanaume wawili na majeruhi 36, ambapo wanne kati yao hali zao ni mbaya na wengine italazimika kuwakata baadhi ya viungo iwapo watashindikana kushonwa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paulo akizungumzia ajali hiyo, amesema chanzo ni mwendo kasi na imetokea majira ya saa 3:30 usiku ikihuhusisha basi la mwisho kutoka jijini Dar es salaam kwenda Morogoro, baada ya dereva wake kufika Lubungo eneo lenye kona na mteremko mkali,na akiwa mwendo kasi, kukutana mbele na lori likiwa na tela, likitokea uelekeo wa Morogoro kuelekea Dar es salaam likiwa linamalizia kupita lori lingine lililokuwa limeegesha barabarani baàda ya kuharibika.
Dereva wa basi aligonga tela la lori hilo lililokuwa kwenye mwendo na kukosa uelekeo na kupindukia bondeni na kusababisha vifo na majeruhi hao...