Jumanne , 26th Jan , 2016

WATU watatu wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi katika matukio tofauti mkoani Geita.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, amesema tukio la kwanza lilitokea Januari 22, mwaka huu, katika kijiji cha Mharamba kata ya Nkome tarafa ya Bugando wilaya ya Geita mkoani humo.

Amesema watu wawili wa familia moja, Pili Juakali (49) na Lucia Juakali (36) wote wa kijiji cha Mharamba mkoani Geita walipigwa na radi wakiwa shambani.

Kamanda Mwabulambo amesema watu hao waligunduliwa na baba yao mzazi, Marco Juakali, wakiwa shambani tayari wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi.

Mwabulambo amesema katika tukio la pili, Flora Malugu (28), mkazi wa mtaa wa Nyakabale, Januari 24, mwaka huu, saa 9 mchana, katika mtaa wa Nyakabale kata ya Mgusu mkoani humo, alifariki dunia baada ya kupigwa na radi kutokana mvua kubwa iliyoambatana na radi.

Awali afisa mtendaji wa kata ya Mgusu, Deus Zabloni, akizungumza na earadio leo eneo la tukio, amesema mwili ya Malugu ulihifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Geita kabla ya kuchukuliwa na ndugu zake, ameacha watoto wanne akiwamo wa wiki mbili ambaye kwa sasa amehifadhiwa katika kituo cha kulea watoto wanaoishi mazingira magumu moyo wa huruma kinachomilikiwa na kanisa Katoliki mjini hapa.

Aidha, Zabloni alisema watoto wengine Grace Boniface (10) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza Nyakabale, Deus (6) na Laghtnnes (3) waliohifadhiwa kwa mjumbe wa eneo hilo.