Jumanne , 17th Mar , 2015

Umoja wa Ulaya nchini umewatunuku tuzo za heshima Watanzania watano mashuhuri, kutokana na mchango wa kila mmoja wao katika kuwaletea Watanzania maendeleo, tuzo zilizotolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka wa maendeleo kwa nchi za Ulaya.

Kutoka kulia ni baadhi ya Watanzania waliotunukiwa Tuzo ya Heshima na Umoja wa Ulaya nchini EU, kutokana na mchango wao katika kuliletea taifa maendeleo.

Waliopata tuzo hizo ni pamoja na mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Dkt Hellen Kijo-Bisimba, aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini balozi Ami Mpungwe, wanamuziki Farid Kubanda (Fid Q) na Khadija Shaban Keysha, pamoja na mchoraji na msanii maarufu Paul Ndunguru.

Akizungumza mara baada ya kupata tuzo hizo, Dkt Hellen Kijo-Bisimba amesema inafurahisha na kutia moyo kuona kuwa mchango wa watetezi wa haki za binadamu unatambulika hata nje ya mipaka ya nchi na kufafanua kuwa hakuna maendeleo mahali pasipo na haki.

Dkt Bisimba amesema kitendo cha yeye kupata tuzo hiyo ya heshima kutoka kwa Umoja wa Ulaya kinazidi kuonyesha umuhimu wa harakati za utetezi wa haki za binadamu, tofauti na ambavyo imekuwa ikidhaniwa kuwa watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakipinga kila jambo linalofanywa na serikali.

Kwa upande wake, mwanamuziki Faridi Kubanda, amesema anajisikia faraja kupata tuzo hiyo ambayo mchango wake anadhani ni jinsi alivyokwenda mbali zaidi ya kufanya kazi ya muziki.

Kwa mujibu wa Kubanda, anakumbuka jinsi alivyotumia sanaa ya muziki kuwakutanisha vijana waliokuwa wanatumia madawa ya kulevya, ambao aliwaweka katika kituo kimoja na kuwafundisha muziki wa Hip Hop, kitendo ambacho kiliwafanya vijana hao waachane na matumizi ya dawa za kulevya.