Shekhe Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mufti wa Tanzania, Aboubakar Zubeir Bin Ally.
Sheikh Zubeir aliyasema hayo jana kwenye mkutano mkuu wa Bakwata uliompitisha kuwa Mufti wa Tanzania kwa kura za wajumbe wote 310 baada ya mtu aliyeingia naye katika ushindani huo kujitoa.
Katika kinyang’anyiro hicho Sheikh Aboubakar alikuwa na wenzake watatu ambao ni Sheikh Khamis Mtupa, Sheikh Hassan Kiburwa kutoka mkoa wa Kigoma na Sheikh Ally Mkoyogole kutoka Dar es Salaam.
Tume ya dini iliyaondoa majina ya masheikh wawili na kuwabakiza Mufti na Sheikh Mkoyogole ambaye naye aliamua kwa hiyari yake kujitoa ndipo wajumbe wakapiga kura za ndiyo.
Katika hotuba yake Mufti aliwataka watanzania kumwomba Mungu ili ailinde nchi ya Tanzania katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais lakini akataka waislamu wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu.
Aidha aliwaagiza masheikh wote wa mikoa, wilaya na kata kuomba dua kwa Mungu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili Mungu aendelee kuidumisha amani ya nchi.
“Kama watu hawaombi Mungu anawaachia tu lakini wakiomba yeye atatenda tena atatenda yaliyomema zaidi,” alisema Sheikh Aboubakar.
Kiongozi huyo aliwashukuru waislamu kwa kumwamini na kumpa kazi ya kuwatumikia na kuahidi kushirikiana nao kwa ajili ya kulijenga baraza la waislamu nchini (Bakwata) na kuwa pamoja katika masuala yote ya maendeleo ya baraza.
Ahadi nyingine kwao ni kuwa hatakuwa mtu wa ofisini na badala yake atatenga muda wa kutembelea mikoa na wilaya ili kuimarisha dini ya kiislamu.
“Ninaliagiza baraza kulinda amani ya nchi na utulivu na kujiepusha na viashirio na kila jambo linalovuruga amani ya nchi hii huku akisema kuwa uislamu ndiyo kitovu cha amani,” alisema Sheikh Mkuu.
Katika hatua nyingine Mufti huyo alimshukuru Sheikh Ally Mkoyogole kwa kumwamini na kumwachia nafasi hiyo na kusema kuwa huo ndiyo ucha Mungu wa kweli.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye alikuwa ni mgeni rasmi Chiku Galawa, aliwataka waislamu kuwakumbusha vijana wao katika kusoma elimu ya dini pamoja na elimu nyingine ili wasipitwe na fursa zilizopo.
Galawa alisema kuwa Quruan inawagiza waislamu kusoma zaidi na kutenda mema lakini wanapaswa kufanya hivyo kwa kuonesha kwa vitendo kile wanachokisoma ili kuleta mabadiriko nchini.
Hata hivyo alionesha masikitiko kuwa alipokea majina mengi kwa vijana waliokamatwa na madawa ya kulevya lakini asilimia 90 ya majina hayo yalikuwa ni ya Kiislamu jambo alilosema linapaswa kutolewa elimu kwa vijana.
Katibu Mkuu wa Bakwata Seleman Lolila aliwataja wajumbe waliostahili katika Mkutano huo ni Masheikh wa Mikoa na wilaya, wenyeviti na makatibu wa halmashauri za Bakwata mikoa na wilaya na Katibu Mkuu.
Mapema asubuhi ya jana ulinzi uliimarishwa kwenye ukumbi wa hotel ya African Dreams uliopo katika Manispaa ya Dodoma ambapo polisi wenye silaha walionekana kulinda eneo lote la hoteli hiyo iliyoko pembezoni mwa mji.
Hata hivyo hali ya utulivu ilikuwa imetawala katika eneo hilo huku baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wakionekana kukaa makundi makundi wakiendelea kujadiliana masuala mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika mkutano huo.
Tukio la kufurahisha zaidi lilikuwa pale wagombea wote wanne wa nafasi ya mufti wa Tanzania walipotoka nje na kukaa katika viti vya pamoja hali iliyowavutia wajumbe wengi pamoja na waandishi wa habari ambao walianza kuwapiga picha kwa ajili ya kumbukumbu ya tukio hilo.
Wasifu wa mufti:
Alizaliwa Juni 20 1953 wilaya ya Korogwe mkoa wa Tanga.
Elimu ya msingi alisoma Korogwe Tanga kabla ya kujiunga na Shule ya Seminari ya St Rafael iliyoko Old Korogwe. Elimu ya dini alisoma kwa Sheikh Abdlrahman Bin Omar na kwa Sheikh Mohamed kisha alisoma elimu ya Sekondari katika kituo cha Shamal Education Center na alisoma kozi maalum katika kituo hicho kuhusu mambo ya lugha akibobea katika lugha ya Kiingereza.
Uzoefu katika kazi
Amekuwa mjumbe wa baraza la Uramaa kwa miaka 22, naibu Kadhi Mkuu namba moja, Naibu Mufti wa Tanzania, Rais wa Islamic Center, Mwalimu wa Masjid ya Mtambani tangu mwaka 1976 hadi 1997, Mwenyekiti wa bodi ya Shule ya Msingi na Mjumbe wa Bodi ya kupiga vita dawa za kulevya Tanzania, ni mufasihi wa Quruan katika Radio ya Jamaled hasa nyakati za siku kuu za dini.
Aliteuliwa kushika nafasi ya kaimu mufti Juni 22 mwaka huu nafasi aliyoishikilia hadi jana alipochaguliwa rasmi.