Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadick.
Mhe. Sadick amesema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha amani wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge baadaye mwaka huu.
Mhe. Sadick ametaja baadhi ya matendo hayo kuwa ni chokochoko za kidini na zile za kisiasa, ambazo mara nyingi vijana ndio wahusika wakubwa wa utekelezaji wa matendo hayo.
Ametaja namna vijana wanavyotumika kuleta chokochoko kuwa ni katika mikutano na harakati za kisiasa ambapo vijana wamekuwa wakitumika kufanya vurugu na kwamba panapotokea maafa wao ndio waathirika wakubwa.
Amewataka watanzania kujenga moyo wa upendo na kuvumiliana, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa akitekeleza jukumu la kudumisha amani miongoni mwa jamii.
Katika hatua nyingine, viongozi wa dini na imani mbalimbali nchini wametakiwa kuwaacha waumini wawe huru kufanya maamuzi wanayoyataka kuhusu kura ya maoni kwa katiba inayopendekezwa.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum, amesema hayo katika mahojiano na Hotmix ambapo amesema kila mtu ana haki ya kufanya maamuzi kuhusu katiba inayopendekezwa na si kwa msukumo kutoka kwa viongozi wa kiimani.
Kauli ya Sheikh huyo wa mkoa wa Dar es Salaam imekuja siku chache baada ya baadhi ya viongozi wa dini nchini, kuwataka waumini wao kuikataa katiba inayopendekezwa kwa madai kuwa ina mapungufu mengi.