Alhamisi , 4th Jun , 2015

Watanzania wametakiwa kujenga tabia pamoja na kuishi maisha ambayo yatawasaidia kuwaepusha dhidi ya majanga mbalimbali yakiwemo yale ya moto, ajali, milipuko ya magonjwa pamoja na mafuriko.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Florence Turuka, amesema hayo leo wakati wa mafunzo kwa watumishi wa ofisi ya waziri mkuu, juu ya namna ya kuzuia na kuepusha madhara yanayoweza kuikumba jamii kutokana na majanga.

Turuka amesema wakati serikali imetunga na kupitisha sheria ya usimamizi wa majanga na dharura ambayo kimsingi inaweka maandalizi ya kuzuia athari za majanga hayo, kuna haja ya wananchi nao kujiweka tayari kuepuka uwezekano wa kukumbwa na majanga hayo.

Kwa upande wake, mdau wa masuala ya majanga na dharura Bw. Amini Hillary Mshana amesema mbinu ya kuzuia majanga kutokea ndiyo njia ya kisasa kabisa ambapo ametolea mfano wimbi la ajali za barabarani zilizolikumba taifa hivi karibuni kuwa zingeweza kuepukika iwapo madereva wangezingatia taratibu bora za uendeshaji vyombo vya moto.

Kwa upande wake, mwezeshaji katika mafunzo hayo, Naima Mrisho kutoka ofisi ya Waziri Mkuu amesema sheria mpya ya kuzuia majanga na maafa inaipa serikali fursa ya kuweka maandalizi ya namna ya kukabiliana na majanga na maafa ambapo amewataka watumishi wa umma kuisoma na kuifahamu sheria hiyo ili kila mmoja afahamu mipaka ya majukumu yake.