Ijumaa , 2nd Jan , 2015

Tume ya Uchaguzi imetangaza tarehe rasmi ya kuanza zoezi hilo kwa nchi nzima kuwa itakuwa ni tarehe 16.02.2015 hadi tarehe 15.03.2015 kwa kanda ambayo tume hiyo itaichagua baadaye kulingana na hali ya hewa itakavyoruhusu.

Jaji mstaafu Damian Lubuva

Jumla ya wananchi 51,721 sawa na asilimia 80.2 ya wananchi 64,510 waliotarajiwa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa kielektronik unaofahamika kama BVR wameandikishwa katika zoezi la majaribio lililoendeshwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika majimbo matatu Tanzania bara.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Damian Lubuva wakati akitoa taarifa ya zoezi hilo jijini Dar es salaam, na kusema kuwa Tume hiyo imebaini changamoto kadhaa katika zoezi hilo ikiwemo ya usalama wa wananchi wanaoandikishwa.

Amesema zoezi hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa kwa sababu matokeo ya jumla yanaonesha kuwa idadi ya wapiga kura waliojitokeza kujiandikisha ilikuwa kubwa na kuvuka malengo ya waliokadiriwa.

Amesema katika mkoa wa Dar es salaam, Kata ya Bunju wapiga kura 15,123 waliandikishwa kati ya 27,148 na kata ya Mbweni wapiga kura 6,200 waliandikishwa kati ya wapiga kura 8,278.

Aidha Jaji Lubuva amesema katika mkoa wa Morogoro, Kata za Ifakara, Kakingiuka, Ipangala, Mlabani na Viwanja Sitini wapiga kura walioandikishwa ni 19,188 wakati makisio yalikuwa ni watu 17,790 .

Katika mkoa wa Katavi Halmashauri ya Mlele kata za Ikuba, Usevya na Kibaoni wapiga kura 11,210 waliandikishwa wakati makisio yalikuwa 11,394.

Amesema matokeo hayo yanadhihirisha kuwa vifaa vya uandikishaji vilifanya kazi vizuri na hivyo vinaweza kutumika katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa ni nzima

Jaji Lubuva pia ametangaza tarehe rasmi ya kuanza zoezi hilo kwa nchi nzima kuwa itakuwa ni tarehe 16.02.2015 hadi tarehe 15.03.2015 kwa kanda ambayo tume hiyo itaichagua baadaye kulingana na hali ya hewa itakavyoruhusu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uchaguzi NEC bwana Julius Mallaba amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekua sio waaminifu katika utoaji wa taarifa na kusababisha zoezi hilo kuenda polepole.

Zoezi hilo la majaribio limefanyika kwa siku 7 katika baadhi ya kata za majimbo ya Kawe mkoani Dar es salaam, Kilombero mkoani Morogoro na wilaya ya Mlele mkoani Katavi.