Sehemu ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwl.Nyerere
Takribani watanzania 5000 wanatarajia kupata ajira ambazo zitazalishwa baada ya kukamilika kwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere uliopo Jijini Dar es salaam ambao unaendelea kujengwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya viwanja vya ndege TAA wakili Ramadhani Maleta amesema hadi kufikia mwakani Desemba 2017ajira hizo zitaanza kutolewa na zitakua kwenye sekta mbalimbali ambazo zitapatikana katika uwanja huo mpya.
Amesema uwanja unategemea kuhudumia ndege za kimataifa 20 kwa wakati mmoja kwakuwa utafungwa vifaa vya kisasa ambavyo vitawavutia wawekezaji kuja nchini kuwekeza na uwanja huo unatarajia kutoa huduma kwa abiria milioni 6 kwa mwaka mmoja wakati uwanja uliopo kwa sasa unahudumia abiria Milioni 2.5 kwa mwaka.
Kwa upande wao viongozi wa dini mbalimbali waliofika kutembelea uwanja huo wamesema ni wakati sasa kwa watendaji wa serikali waache kuiba pesa ambazo zinatolewa na serikali kwa lengo lakuboresha miundombinu nchini.
Ukarabati huo unatarajia kugharimu shilingi bilioni 500.





