Ijumaa , 4th Sep , 2015

Kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu nchini utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu, wanasiasa nchini wametakiwa kuwa na ajenda za kulinda na kutetea uhifadhi ili kuwa na utalii endelevu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Afisa Habari wa Tanapa ,Pascal Shelutete wakati akizindua kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani

Hayo yameelezwa na Afisa Habari wa TANAPA, Pascal Shelutete wakati akizindua kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani itakayodumu kwa miezi sita huku ikilenga watanzania laki tano kutembelea hifadhi ikiwemo Tarangire, Manyara, Ngorongoro na hifadhi nyingine za taifa ili kujionea utajiri wa rasilimali wanyamapori na misitu iliyopo Tanzania.

Shelutete amesema kuwa wagombea wa urais na ubunge wanapaswa kuweka uhifadhi katika ilani zao za vyama ili kulinda uhifadhi ambao unaongoza katika kuchangia pato la taifa nchini.

Meneja Masoko wa TANAPA, Victor Kentasi amesema kuwa katika kipindi hicho cha kampeni kutakuwa na punguzo kwa makundi yote kuanzia watoto hadi watu wazima pamoja na zawadi mbalimbali ambazo watanzania watapatiwa pindi watakapotembelea hifadhi.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha waongoza watalii TATO, Cyril amewataka watanzania kutumia fursa zilizoko katika sekta ya utalii na kuwekeza na kunufaika na sekta hiyo licha ya kutembelea.

Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na rasilimali za asili za wanyamapori na mimea duniani ikiongozwa na Brazil,Watanzania wanapaswa kutembelea hifadhi na vivutio vya utalii badala ya kutegemea watalii kutoka nje ya nchi.