Jumanne , 15th Jul , 2014

Taasisi na asasi zinazotoa msaada wa kisheria nchini Tanzania zimetakiwa kusogeza huduma za msaada wa kisheria katika magereza na mahabusu mbali mbali nchini, mahali ambako kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria.

Naibu waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania Bi. Angela Kairuki (kushoto).

Naibu waziri wa katiba na sheria Bi. Angela Kairuki amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea ofisi za chama cha wanasheria Tanganyika TLS kama sehemu ya ziara ya kutembelea idara na taasisi zilizo chini ya wizara ya katiba na sheria.

Kwa mujibu wa naibu waziri Kairuki, idadi kubwa ya Watanzania wanaotumikia vifungo na wanaosubiri hukumu, hawafahamu sheria, hatua aliyosema inahitaji huduma za msaada wa kisheria kwa ajili ya kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya kusikilizwa na kuhudumiwa kama inavyoeleza ndani ya katiba.

Naye makamu wa Rais wa TLS, mwanasheria Flaviana Charles amesema kwa kulitambua suala hilo wameanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa watoto na katika kanda za mikoa.

Wakati huo huo, serikali imetenga zaidi ya shilingi billion tisa kwa ajili ya kujenga barabara za halmashauri zote zilizoko katika mkoa wa Dodoma.

Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli amesema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kujengea barabara zilizoko katika halmashauri za mkoa wa Dodoma ambapo zimetoka kwenye mfuko wa barabara na kuwataka viongozi wa mkoa huu kuzitumia fedha hizo kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk, Rehema Nchimbi amempongeza dr Maghufuli kwa utendaji kazi wake na kutaka kasi ya Maghufuli iende sambamba na kasi ya uwekaji taa katika barabara zinazoenda kwenye makazi ya viongozi yaliyoko mjini Dodoma.
...........................