Alhamisi , 8th Feb , 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi katika maeneo hatarishi hususani ya mabondeni waondoke ili kupunguza maafa yanayoweza kusababisha  mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua hizo inarudishwa ili wananchi waendelee na shughuli zao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 8, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imejipangaje kibajeti kurudisha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wahakikishe wanafuatilia maeneo yaliyoathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na wafanye ukarabati wa kurejesha miundombinu iliyoharibika zikiwemo barabara na madaraja.