Alhamisi , 5th Sep , 2024

Wanaume kutoka mitaa mbalimbali mkoa wa Dar es Salaam, wameitaka Serikali kuweka adhabu ya kunyongwa hadharani kwa watu watakaokutwa na hatia ya ubakaji au ulawiti ili kuweza kukomesha vitendo hivyo.

Wanaume waandamana ofisi za mtandao wa jinsia (TGNP)

Wanaume hao wameandamana kwenye ofisi za mtandao wa jinsia TGNP jijini Dar es Salaam, wakiishinikiza Serikali kuchukulia matukio ya ukatili ni ya dharura ikiwezekana kesi ziwe zinasomwa mara moja baada ya tukio kutokea.
“Tumechoka kudhalilishwa na wanaume wenzetu sasa hivi hatuombi tena Serikali bali tunaitaka itunge sheria kali kwa watu wataogundulika wamefanya wanyongwe hadharani ili wengine wenye nia ya kufanya hivyo waogope”, Bushiri Selemani,Mkazi wa Kitunda.
“Sasa hivi hali imekuwa mbaya sana kila kukicha tuasikia kwenye vyombo vya habari kuwa kumetokea ukatili kwani vyombo vya Sheria viko wapi na vinafanya nini hasa tunataka Rais aseme neno kwenye swala hili”, Mahemba Kumbata, Mkazi wa Kitunda.
“Sasa hivi baba wa mtoto haaminiki tunaenda wapi, Tanzania ilikuwa inasikika nchi ya amani lakini sasa hivi watoto wetu hawapo salama na Serikali hatuoni ikichukua hatua kwa wanaofanya hivyo”, Erasto Basil, Mkazi wa Dar es Salaam.

Kwa upande wake mkuu wa idara ya ujenzi wa nguvu za pamoja na haraka pamoja na idara ya utafiti na uchambuzi kutoka mtandano wa jinsi (TGNP), wamekemea vikali matukio ya ukatili likiwemo la baba kwa mtoto wake.
"Kwa namna gani tutakubaliana kwa pamoja kuweka sheria kuwa kali zioneshe hata mfano ikioneshwa hata kwa mmoja wengine waogope, ikiwezekana wanaume wakutane wajue tatizo liko wapi kwanini wanafanya vitendo hivyo", alisema Flora Ndaba, Kaimu mkuu wa idara ya ujenzi wa nguvu za pamoja na haraka.
"Tusisikie jamii yetu ya Tanzania bado kuna ukatili, jamii yote ya Tanzania tukubaliane kwa pamoja tuwalinde watoto kuanzia ngazi ya familia mpaka kwenye jamii tuwalinde watoto wet ili waweze kuishi kwa usalama", alisema  Zainab Mmary, Idara ya utafiti na uchambuzi.

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi amesema wamechoshwa na vitendo hivyo ni wakati wa Serikali kutoa tamko.
"Hatua zisipo chukuliwa hata binadamu ana kiwango cha kuvumilia, sisi tunasema inatosha hatua zichukulliwe kwa watu wanaofanya vitendo hivyo, mfano leo tu asubuhi kuna mtoto amelawitiwa na baba yake na sasa hivi ameachiwa huru sasa yule mama kaja hapa analia anaomba msaada, kwahiyo hiyo pia Serikali, Jeshi la Polisi, watu wote wanaohusika na ulinzi na usalama wanatakiwa walione hili kama dharura",alisema Liundi.