Alhamisi , 24th Mar , 2016

Serikali imewakumbusha Wananchi wa Tanzania kujitokeza kwa wingi kufanya usafi wa mazingira nchi nzima kwa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kuitikia wito wa Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, aliouanzisha tarehe 09 Desemba 2015.

Waziri wa nchi Ofisi ya rais TAMISEMI, Mhe. George Simbachawene,

Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari Waziri wa nchi Ofisi ya rais TAMISEMI, Mhe. George Simbachawene amewataka Viongozi wa makundi yote katika jamii kuwa mfano katika zoezi hilo jema.

Mhe. Simbachawene amesema kuwa mbali ya kwamba kufanya usafi kuna fanya mazingira yapendeze na kuondoa magonjwa yanayo sababishwa na uchafu lakini pia zoezi la kufanya usafi kwa pamoja lina jenga Umoja na Mshikamano wa kitaifa, na kuondoa matabaka ndani ya jamii yetu.

Waziri huyo amewataka watanzania wote kushiriki kikamilifu kufanya Usafi wa Mazingira kwenye Makazi yao, Maeneo ya Biashara, maeneo ya Taasisi za Umma na maeneo yenye mikusanyiko ya watu mbalimbali kama masokoni na minadani na kutaka kila Mtanzania Kujitokeza kufanya usafi bila kujali uwezo wa mtu,hadhi yake,cheo chake, au nafasi yake katika jamii.

Aidha ametumia Fursa hiyo kuwataka watanzania wote wa Mijini na Vijijini kujenge desturi ya kuweka mazingira katika hali ya usafi wakati wote na katika jambo hilo kila mmoja awe mlinzi wa kukemea watu wenye tabia za kutupa taka hovyo ili maeneo yawe katika hali ya usafi na yakuvutia wakati wote.