Jumanne , 21st Jun , 2022

Mkuu wa mkoa wa Mara Ally Hapi, ametoa saa 48 kwa Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka, kupeleka Mganga wa Afya katika Zahanati ya Oliyo iliyopo Kata ya Rabuori pamoja na kuweka ulinzi  kufuatia wananchi kugomea kutumika kwa kituo hicho kwa madai ya kuhitaji kituo cha Afya na sio zahanati.

Mkuu wa mkoa wa Mara Ally Hapi

Amebainisha hayo wakati akizungumza na wazee wa mkoa pamoja na wazee wa kimila ambapo amesema zahanati hiyo ilianza ujenzi kwa nguvu za wananchi na serikali ilimalizia kwa kutoa fedha kiasi cha milioni 50 na ujenzi kukamilika lakini kuwepo kwa mgogoro wa ujenzi wa kituo cha Afya ndani ya Kata hiyo kunapelekea baadhi ya kugomea kuanza kutumika kwa zahanati hiyo.

"Sasa natoa saa 48 huduma za kiafya zianze kutolewa katika zahanati hiyo na yoyote atakayefanya fujo kwa mganga wa afya ama mwananchi watakaoenda kupata huduma kituoni hapo hatua za kisheria zitachukuliwa, tusinyime wananchi huduma kwa sababu ya ulafi wa madaraka kwa watu wachache, " amesema RC Hapi.