
Mwl. Faraja Kristomus
Akizungumza kwenye SupaMix ya East Africa Radio, Mwl. Kristomus amesema asilimia kubwa ya wanafunzi wanapata mkopo lakini wamekuwa wakiutumia vibaya, matokeo yake huisha mapema na kuanza kusota namna ya kujikwamia kiuchumi.
"Taasisi zinazohusika zingeweka jitahada za kuwaelimisha namna ya matumizi mazuri ya fedha za mkopo, lakini pia hata wazazi wana wajibu pia wa kuwaonya watoto wao na kuwafundisha kabla ya kuja chuo, wawaambie kuwa ukienda shule usiwe na matumizi makubwa yanayozidi 8,500 (ambayo wanapewa kwa siku) ", alisema Mwl. Kristomus.
Mhadhiri huyo aliendelea kwa kusema kuwa tatizo hilo limekuwa ni kubwa kwa wanafunzi wengi, ambalo pia ndicho chanzo cha matatizo mengi kwa wanafunzi hao wanapoishiwa, ikiwemo kujiingiza kwenye vitendo viovu na kufeli kimasomo, na kumsababishia matatizo ya kisaikolojia.
"Mtoto kama atalenga kwa 8,500 kwa matumizi mazuri, anaweza aka'survive, lakini wengi wao wamekuwa wakitumia ndivyo sivyo na matokeo yake akiishiwa anaanza kutafuta vyanzo vingine vya mapato, kama ni binti atatafuta mtu wa kumsaidia (mpenzi), atakuwa na maendeleo duni na kumpelekea kushuka kimasomo", alisema Mwl. Kristomus