Jumatano , 4th Dec , 2019

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya REPOA umebaini kuwa wanafunzi wengi wanaosoma katika Vyuo vya Ufundi Stadi, hawana elimu ya kutosha na wengi wao ni wale, waliofanya vibaya kuanzia Shule ya Msingi na hata Kidato cha 4, hali inayopelekea elimu yao kutokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Akizungumza leo Novemba 4, 2019, Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt Lucas Katera, amesema kuwa utafiti huo umefanyika muda wa miaka miwili, kuanzia 2018 hadi 2019, uliokuwa unaangalia suala zima la ajira kwa vijana na mchango wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika kuongeza ajira kwa vijana na kubaini kuwa hata walimu katika vyuo hivyo wako wachache na wengi wao hawana elimu ya kutosha.

"Wengi wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo wanakuwa na elimu ndogo sana ya Msingi na waliofika Sekondari ni wale waliofeli, kwahiyo kutokana naa elimu duni waliyonayo wanashindwa kufuatilia vizuri masomo yao na elimu inayotolewa haikidhi vigezo vya kuingia kwenye soko la ajira, Vyuo hivyo pia vina idadi ndogo ya walimu, lakini pia hawana elimu ya kutosha" amesema Dkt Katera.

Aidha ushauri umetolewa kwa waajiri pamoja na Vyuo Vya Ufundi kuwa na mawasiliano ya pamoja ili kujua ni aina gani ya mitaala ya elimu, inayopaswa kutolewa na yenye kukidhi mahitaji ya soko la ajira kwa vijana