Ijumaa , 11th Dec , 2020

Wizara ya Elimu nchini Kenya, imelazimika kuifunga shule ya kitaifa ya wasichana ya Lugulu, baada ya wasichana hao kuandamana wakilalamikia dhulma ya kimapenzi wanayodai kufanyiwa na walimu wao kiume.

Shule ya Sekondari Lugulu iliyoko nchini Kenya.

Wasichana hao wote wa kidato cha nne katika shule hiyo walitoa malalamiko yao kupitia maandamano ya amani, wakisema kuwa wamechoshwa na tabia za baadhi ya walimu wa kiume wanaodaikuwa wanawadhulumu kimapenzi, na kutaka asasi husika kuingilia kati na kuwanusuru, kutokana na mienendo hiyo ambayo wanadai imekuwa ikiendelea kwa muda sasa.

Mara baada ya shule hiyo kufungwa na wanafunzi  hao kutakiwa kwenda nyumbani, Shirika moja nchini Kenya, lisilokuwa la kiserikali la pambazuko la wanawake limetaka uchunguzi wa kina kufanywa kuhusiana na madai ya ubakaji yaliyotolewa na wasichana wa shule hiyo, huku wakizitaka idara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu, kuharakisha uchunguzi na kutoa ripoti, ili waliotekeleza vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.