Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Waziri Simbachawene ametoa muda wa siku sita kwa serikali za mikoa kuwasilisha taarifa za hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi wa serikali waliosababisha matumizi mabaya ya fedha na kuwaingiza walengwa wasiostahili kwenye mpango wa kuondoa Kaya masikini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Simbachawene ametoa agizo hilo kwenye hotuba yake iliyosomwa leo na mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla aliyemwakilisha kufungua Mkutano wa Siku mbili wa Kazi wa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka wa Serikali za Mitaa wa Mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Ruvuma na Songwe.
Kupitia hotuba hiyo, Simbachawene amesema kumekuwa na Changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) na kuzitaja miongoni kuwa ni pamoja na Kuingizwa kaya zisizo na sifa,kuachwa kwa kaya ambazo ni masikini zaidi na Familia za Viongozi kuingizwa kwenye mpango.
Nyingine ni Kutofikisha ruzuku stahiki kwa walengwa wa mpango kutokana na baadhi ya watumishi wa umma au wasimamizi wasio waaminifu kupunguza malipo kwa walengwa,Kuchukua malipo ya walengwa waliofariki au kuhama kutoka kwenye maeneo yao na baadhi ya walengwa kutofika wao wenyewe kupokea fedha na badala yake wengine wamekuwa wakichukuliwa fedha kitu ambacho si utaratibu.
Amesema wapo pia viongozi wa Kamati za Mpango ambao nao wamejiweka kuwa sehemu ya walengwa jambo alilosema haliruhusiwi.
Simbachawene amesema kufuatia utekelezaji wa agizo la TAMISEMI kupitia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora la Februari 2016 la kufanya uhakiki wa kaya zilizopo kwenye mpango ili kuziondoa zisizo na sifa, mpaka sasa kaya 32,456 zimeondolewa kwenye mpango huo.
Amesema kati ya kaya hizo 9,342 ni za watu wasiofahamika na kutojitokeza, kaya 8,348 ni za wasio na sifa,7,819 ni za waliofariki, kaya 2,999 ni za viongozi na kaya 3,948 ni za waliohama sehemu ambapo mpango haujaanza.




.jpg?itok=0CrdpE0P)