Jumamosi , 24th Sep , 2016

Mahakama ya hakimu mkazi Bukoba imewatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha maisha watu watatu waliokuwa na tuhuma ya kuhusika na vitendo vilivyokuwa vimekithiri mkoani Kagera mwaka jana vya uchomaji wa makanisa katika maeneo mbali mbali mkoani humo.

Akisoma hukumu hiyo iliyotolewa jana hakimu mkazi wa mahakama hiyo Victor Bigambo, alisema mahakama imetoa adhabu hiyo kwa Ngesella Joseph, Rashid Mzee na Ali Dauda baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Mwendesha mashtaka wa serikali, Emmanuel Mavelle alisema watu hao mashtaka yaliyowatia hatiani kuwa ni ya kula njama na kuchoma makanisa, pia amesema watu hao wanakabiliwa na mashtaka mengine ya kuua watu kwa kuwakata watu koromeo, ambayo yanasikilizwa na mahakama kuu kanda ya Bukoba.

Kamanda wa jeshi la polisi katika mkoa wa Kagera kamishina msaidizi mwandamizi Augustine Ullomi aliyekuwa mahakamani wakati hukumu ikitolewa, amewaomba wananchi waendelee kuwafichua wahalifu ili jeshi hilo liweze kukabiliana nao.