Jumatatu , 20th Mar , 2023

Wakazi wa kijiji cha Makarwe kata Buleza halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wameilalamikia halmashauri ya wilaya hiyo kuwanyang'anya ardhi yao ambayo ilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu uliokuwa ukitumiwa na vijana wa kijiji hicho na eneo hilo kupimwa viwanja vya makazi

Wakizungumza na EATV wakazi hao wamesema kuwa wamepewa uwanja huo na serikali ya kijiji tangu mwaka 2001 na kuanza kuutumia kuchezea mpira wa miguu, lakini halmashauri walipoanza upanuzi wa mji waliwanyang'anya uwanja wao bila kuwashirikisha. 

"Sisi hatuwezi kuzuia halmashauri kutujengea uwanja mwingine endapo wataamua kutumia huo uwanja kuweka viwanja vya makazi, tunachotaka kama tunajengewa uwanja mwingine tupewe hati milki, lakini pia tusije tukajengewa uwanja ambao msimu wa mvua utajaa maji, maana eneo tunakoambiwa utahamishiwa linajaa maji na lina mwamba" tunahofia baadae vijana kukosa sehemu ya kuchezea" amesema Mwenyekiti wa Kijiji. 

Akitoa ufafanuzi kwa njia ya simu, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Elias Kayandabila, amekiri maeneo hayo kupimwa kwa ajili ya kupanua eneo la mji, lakini akadai kuwa wamekwishapima kiwanja kingine kipya cha mpira, ambacho muda wowote mkandarasi ataanza kazi ya kusawazisha, na kuwa kiwanja hicho kitakuwa bora zaidi kuliko cha awali. 

"Vijiji vyote vipo chini ya halmashauri, kwa hiyo hata kiwanja hicho tayari kimepimwa na kina hati, na hati hiyo hawapewi wanakijiji bali kitapewa kijiji, maeneo yote ya wazi ni mali ya serikali na sio ya mtu binafsi, kwa hiyo wananchi niwaombe wawe watulivu wakati suala hili linatafutiwa ufumbuzi" amesema Kayandabila.