Jumanne , 6th Jan , 2015

Wakulima wa mpunga Mkoani Mbeya wameshauriwa kukata Bima ya Mashamba yao ili kuepuka hasara wanayoweza kuipata punde mazao yao napoharibika kwa ukame, viwavijeshi au majanga mengine yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda alipotembela Mashamba ya mpunga Mkoani Mbeya

Akitoa elimu juu ya kilimo cha mkataba, kwa ajili ya wakulima wa mpunga wa kata ya Chitete wilayani Momba kupewa mbegu na pembejeo za kilimo ili waweze kuzalisha mazao bora yanayokidhi mahitaji ya soko, mkurugenzi wa kampuni ya mtenda kyela rice, George Mtenda amewashauri wakulima hao kuhakikisha wanakata bima ya mashamba yao ili inapotokea wakashindwa kuvuna kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa waweze kufidiwa gharama zao.

Afisa ughani wa kata ya Chitete, Samson Mwasote amesema kuwa wakulima wengi wa kata hiyo wamekuwa wakilima bila kutumia mbolea wala ushauri wa kitaalam kutokana na kukosa uwezo wa kiuchumi wa kupata pembejeo, hivyo wakisaidiwa kwa kupewa mbegu bora na pembejeo wataongeza uzalishaji mara dufu

Baadhi ya wakulima wamesema kuwa utaratibu wa kukata bima ya mashamba yao ni mzuri na utawasaidia kulima kwa kujiamini na bila woga wa kuzikimbia familia zao punde wanapopata hasara wakiogopa kulipa madeni ya pembejeo walizokopeshwa.