Jumatano , 4th Mei , 2016

Wakulima katika kijiji cha Sakalilo kata ya Ilemba wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, wameombwa kupanuliwa kwa wigo wa Utoaji Elimu ya kilimo cha kisasa katika zao la mpunga ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Kilimo cha Mpunga

Elimu wanayohitaji kuongezewa ili kuwafikia wakulima wengi zaidi ni pamoja na ya Kilimo Shadidi inayotajwa kuwa na faida kubwa kwa kuongeza uzalishaji katika zao la Mpunga.

Hayo yamebainishwa na wanachama wa kikundi cha Sakalilo Amcos cha kijijini Sakalilo wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa,walipokuwa wakielezea Mafanikio waliyoyapata kufuatia Elimu ya Kilimo Shadidi waliyopewa kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Uholanzi la SNV.

Wakizungumza na Wanahabari kutoka shirika la Wanahabari la Elimisha,wanachama hao walisema kupitia Kilimo Shadidi wameweza kuongeza uzalishaji wa zao la Mpunga kutoka Magunia matano hadi saba kwa Ekari na kufikia Gunia 15 hadi zaidi ya 20 kwa eneo hilo hilo.

Mwenyekiti wa Sakalilo Amcos, Osphard Sinkala, na mwanachama wake Elizabert Mgazi,wamesema awali walikuwa wakivuna mazao kidogo licha ya kutumia gharama kubwa tangu maandalizi ya shamba,kupanda hadi kuvuna.

Wamesema kupitia kilomo shadidi wameweza kutumia mbegu kidogo,kupata urahisi wa kuhudumia shamba hususani kwa kazi za palizi na matumizi kidogo ya maji huku wakitarajia mavuno mengi.

Hata hivyo Afisa ugani wa kijiji hicho,Robert Kasunga amesema Elimu zaidi inahitajika kwa wakulima wengine ili waweze kuondokana na kilimo cha mazoea kisicho na tija.