Baadhi ya wakimbizi kutoka Somalia wakila kiapo
Serikali imewaonya baadhi ya wakimbizi wa kisomali waliopewa uraia nchini kuacha kupandikiza mbegu za ugaidi kwa watanzania na badala yake wanapaswa kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa ili kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu iliyosababisha mamlaka husika kuwapatia uraia wa kuishi nchini.
Agizo hilo limetolewa na waziri wa mambo ya ndani mheshimiwa Mathias Chikawe wakati wa hafla fupi ya kuwapatia hati za uraia wakimbizi wapatao 1514 raia wa Somalia waliokuwa wamehifadhiwa katika kambi ya wakimbizi iliyopo eneo la Chogo wilayani Handeni.
Amesema vipo baadhi ya vikundi vinavyohusishwa na ugaidi vimekuwa vikiingia nchini kwa mbinu mbalimbali zikiwemo za kidini na biashara hivyo ni jukumu la wakimbizi waliopewa uraia kwa kushirikiana na wenzao kuhakikisha wanalinda amani kwa sababu usalama unaanzia kwao kabla vyombo vya dola havijaingilia kati.
Wakijibu agizo hilo la mheshimiwa Chikawe, kupitia kwa mwakilishi wa wakimbizi waliopewa uraia Bwana Saad Abdulrahman wamemhakikishia waziri kuwa watadumisha amani na wameomba awapelekee salamu kwa mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Jakaya Kikwete kuwa watakuwa mabalozi wa kulinda amani nchini.
Kufuatia hatua hiyo, mwakilishi wa shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) nchini Bibi, Joyce Minds-Coll, amesifu jitihada za serikali ya Tanzania kwa kuwapa hifadhi wakimbizi wa nchi ya Somalia.
Wakimbizi hao, wengi wao walitokea katika wilaya ya Handeni na Bagamoyo ambao vizazi vya karne ya 19 vilichukuliwa kama watumwa na kupelekwa katika nchi ya Somalia kwa ajili ya kutumikishwa.