Hatua ya wananchi wa jamii ya Wamasai na Wasonjo ya kukubaliana kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo na kufichua mtandao unaoingiza silaha za kivita katika maeneo yao imeungwa mkono na wafugaji wa wilaya ya Narock nchini kenya.
Wafugaji hao wamepongeza hatua hiyo kwakuwa silaha hizo hutumika kuua wananchi wasio na hatia na wameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali.
Kiongozi wa mila wa wafugaji wa wilaya ya Narock Bw Nicholaus Kiripesi amesema muafaka wa wamasai na wasonjo uliofikiwa unahitaji kuungwa mkono sio tu na wananchi wa jamii hizo bali hata wa jamii nyingine na pia viongozi wa kada mbalimbali.
Amesema kama wafugaji hao wa Tanzania wakiweza kudumisha makubaliano waliyofikia ya kuondoa tofauti zao, suala la kukabiliana na mtandao wa watu wanaoingiza silaha litakuwa rahisi na ni jambo linalowezekana.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Wamasai na Wasonjo Bw Rafael Long'oi na mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Bw Elias Wawalali wamewataka wananchi wa pande zote mbili kuunga mkono jitihada za wazee wa mila za kudumisha makubaliano hayo kwa kuendelea kuwafichua wanaomiliki silaha na kwamba watakaosalimisha hawatachukuliwa hatua yoyote.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya jamii za wamasai na wasonjo, wananchi wakiwemo vijana wa jamii hizo walikula na kucheza pamoja hali inayoonesha kumaliza tofauti zao.