Ijumaa , 25th Jul , 2014

Raia wawili kutoka nchi kenya wamehukumiwa miaka 20 kila mmoja na mahakama ya wilaya ya Tarime mkoani Mara nchini Tanzania baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyara za serikali.

Watuhumiwa hao walikutwa na nyara za serikali ikiwemo meno ya tembo, ngozi ya chui, vipande vya nyama ya wanyama pori na nyaya za kutegea wanyama pamoja na darubini.

Hakimu aliyeotoa hukumu amesema adhabu iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kuhujumu hifadhi za taifa ambazo ndio tegemeo kwa uchumi wa taifa.

Katika hatua nyingine, wakala wa Mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka DART umewataka wafanyabiashara jijini Dar es salaam nchini Tanzania wanaotumia maeneo yaliyojengwa kwa ajili ya watembea kwa miguu na baiskeli kuondoka kabla hawajachukuliwa hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa usafirishaji na mpango wa DART Mhandisi Serapio Tigahwa amesema kuwa serikali haimkatazi mtu kufanya biashara kama atazingatia maeneo yaliyotengwa.

Aidha Tigahwa amesema kuwa imebaki miezi michache ili mradi huo ukabidhiwe na kuanza kutoa huduma kwa wakazi wa jijini Dar es salaam.