Jumatatu , 11th Jan , 2016

Wananchi waishio kijiji cha Nasholi kata ya Kikatiti wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wamelalamikia kero ya uhaba wa maji inayowakabili na kuathiri shughuli za kijamii hivyo wameiomba serikali itatue kero hiyo ili kukidhi uhitaji huo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nasholi Robert Akiyoo

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao Nurueli Mbise na Rose Jackson wamesema kuwa wamekua wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji pamoja na kushinda katika mabomba ya maji ambapo maji hupatikana kwa shida hivyo kusimamisha kazi zao kwa muda mrefu

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nasholi Robert Akiyoo amesema kuwa kwa sasa wamepeleka maombi ya kuunganishwa katika bomba kuu la maji badala ya kupata maji ya mgao ambayo huwafikia wananchi wachache licha wananchi wengi kuhitaji huduma hiyo ya maji.

Diwani wa Kikatiti Elisa Mungure akizungumza katika mkutano wake wa kuwashukuru wananchi amewataka viongozi na wananchi kushirikiana kutafuta njia za kupata vyanzo vya maji mbadala ikiwemo kuchimba visima ili kukidhi uhitaji mkubwa wa maji unaowakabili wananchi walio wengi.

Changamoto ya maji hasa katika maeneo mengi ya wafugaji huzorotesha juhudi za wananchi kujitafutia maendeleo ya kijamii na kiuchumi na wakati mwingine husababisha njaa na milipuko ya magonjwa.