Jumanne , 3rd Nov , 2015

Wananchi wa kijiji cha Nayobi wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wamelalamikia kero ya uhaba wa maji inayowasababishia kukesha kwenye bomba la kijiji kwa siku tatu wakisubiri maji jambo linalopelekea shughuli za kijamii na kiuchumi kusimama.

Mwenyekiti wa Kijiji Naiyobi Meleji Sikoni

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa kwa muda mrefu wamekua wakiteseka kupata huduma za maji huku kinamama wajawazito wakijifungulia bombani apo baada ya kukaa kwa muda wakitafuta maji huku wengine wakilazimika kukesha na watoto wadogo.

Mwanakijiji John Lomnyaki amesema kuwa kwa sasa wanakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji pamoja na chakula na hata pale wanapopata chakula hukosa maji ya kupikia chakula hicho na kuziacha familia zao zikitaabika kwa njaa.

Kesia Laizer amesema kuwa wamekuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji na wakati mwingine kulazimika kukesha kwenye bomba hilo la maji wakisubiri huduma hiyo muhimu ya maji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji Naiyobi Meleji Sikoni amesema kuwa kwa muda wa miaka 20 wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji hivyo ameiomba serikali na mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iwasaidie kutatua tatizo hilo sugu linalowaathiri wananchi wengi.

Wilaya ya Ngorongoro inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji pamoja na chakula hasa katika kipindi hiki cha kiangazi, juhudi zinahitajika kwa upande wa serikali na mamlaka ya Ngorongoro ili kuweza kuwanusuru wananchi na baa la njaa pamoja na uhaba wa maji.