Jumapili , 23rd Nov , 2014

Zaidi ya wakazi Hamsini wa eneo la Loliondo wilaya ya Ngorongoro nchini Tanzania, wamesafiri hadi jijini Dar es Salaam, ambako wamefanya maandamano ya amani.

Mkazi wa Loliondo akiwa amebeba moja ya mabango yanayoeleza kupinga mpango wa serikali wa kutaka kuchukua eneo lao katika kile wanachokiita kuwa ni kukiuka taratibu na sheria ya ardhi. Kushoto kwake ni mmoja wa wakazi wa Loliondo ambaye pia ni Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Bw. Onesmo Olengurumwa.

Maandamano hayo ni ya kupinga kile walichokiita kuwa ni mpango wa wizara ya maliasili na utalii wa kutaka kugawa eneo lao linalozunguka mbuga ya wanyama ya Serengeti na hifadhi ya wanyamapori ya Ngorongoro kinyume na sheria.

Wakizungumza kwa uchungu mbele ya waandishi wa habari, wakazi hao wamesema mpango huo unaoonekana kuratibiwa na waziri wa maliasili na utalii mheshimiwa Lazaro Nyalangu, unaenda kinyume na agizo alilolitoa waziri mkuu Mizengo Pinda mwaka jana ambapo alitaka mamlaka kamili ya eneo hilo yaende kwa wakazi wa Loliondo.

Wakazi hao ambao wameandamana na wazee wa kimila wa kabila la kimasai maarufu kama ‘Laigwanani’, wamesema inashangaza kuona waziri Nyalandu anataka kutwaa eneo lao na kuligawa kwa mwekezaji kwa kisingizio kuwa uwepo wao unasababisha uharibifu wa mazingira, madai waliyosema kuwa siyo ya kweli.

Wameongeza kuwa tofauti na inavyodhaniwa kuwa uwepo wao utasababisha uharibifu wa mazingira, wakazi hao wamesema wao ni watunzaji wazuri wa maliasili za misitu wakiwemo wanyama, na kwamba, hali hiyo inathibitishwa vizuri na jinsi eneo  hilo lilivyoendelea kuwa na utajiri wa maliasili za misitu kwa kipindi chote hiki, tofauti na maeneo mengine ya nchi ambako wanyama na misitu vimetoweka na hata ardhi kugeuka jangwa.