Ijumaa , 14th Mei , 2021

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amesema mtu yeyote anayekusudia kufanya maasi katika siku ya Eid anadhihirisha ni kwa jinsi gani alikuwa hajafunga bali kushinda njaa kwa siku 30.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha East Africa Radio Sheikh Alhad amesema uaminifu uliokuwepo katika kipindi chote cha mfungo wa  Ramadhani unatakiwa uendelezwe katika shughuli zote na maisha kwa ujumla.

"Muislamu anatakiwa kuyaendeleza aliyojifunza katika mwezi wa ramadhani, mtu ambaye amejipanga kufanya maasi siku ya Eid, huyu ni mtu ambaye anaonyesha dalili kwamba funga yake ilikuwa ni patupu, alikaa tu na njaa muda wote wa siku 30" amesema Sheikh Alhad 

"Sisi waislamu hatutakiwi tujipange kwa ajili ya kutenda maasi kwa ulevi, au kwa matendo machafu mbalimbali, ni jambo lisilofaa na linaonesha watu hawajaelewa lengo na dhumuni la mfungo wa ramadhani" aliongeza Sheikh Alhad

Akizungumzia namna ya kusherehekea sikukuu hii ya Eid al-fitr, Sheikh Alhad amewataka waislamu kusherehekea kwa kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuwasisitizia wazazi kuwapeleka watoto katika maeneo salama na yasiyo hatarishi.                                                                                                        

"Namna ya kusherehekea ni kwa kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu, watu waende maeneo yanayofaa, tuwapelekee watoto wetu maeneo salama na si hatarishi, mabinti wetu wasichaganyike na wavulana katika fukwe na kurudi saa nne usiku," amesema Sheikh Alhad