WAHAMIAJI haramu 305 wamekamatwa na idara ya uhamiaji mkoani Shinyanga katika kipindi cha kuanzia mwenzi Januari hadi Desemba mwaka 2014 kutokana na ushirikiano mzuri na jamii, huku kati yao 75 walifikishwa mahakamani na nchi ya Burundi ikitajwa kuongoza.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake afisa uhamiaji mkoa wa Shinyanga Bi. Annamaria Yondani, amesema kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu kumetokana na juhudi za utoaji elimu katika jamii kuwafichua watu ambao wana mashaka nao kuwa siyo raia wa Tanzania.
Amesema kati ya wahamiaji haramu 305 walitoka katika mataifa mbalimbali ambapo nchi ya Burundi inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji 127, na waliofukuzwa nchini kati yao ni 64 huku waliofungwa ambao wanatoka nchi hiyo ni 21.
Amefafanua kuwa wahamiaji haramu wengine wanatoka Brazili, Pakistani, Zimbabwe, Kenya, India, China na Congo , walihojiwa na hatua mbalimbali za kisheria zikachukuliwa dhidi yao kutokana na kuingia nchini bila kuwa na kibali cha kuishi nchini.
Bi. Yondani amesema idara ya uhamiaji ina mkakati wa kutoa semina elekezi kwa viongozi wa vijiji,mitaa,vitongoji na kata kwa waliochaguliwa hivi karibuni, kwa kushirikiana na maafisa uhamiaji kata ambao walikuwa wakitoa elimu awali na kuwasisitiza viongozi pindi kuwafichua wahamiaji haramu.