Alhamisi , 11th Feb , 2016

Wahamiaji haramu 24 kutoka nchini Burundi watiwa mbaroni mkoani Mara.

Idara ya uhamiaji katika mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, inawashikiria wahamiaji haramu 24 raia wa nchi ya Burundi, ambao wamedai kutoroka kutoka moja ya kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya kwa madai ya kuhofia usalama wao katika kambi hiyo.

Afisa uhamiaji wa kituo cha Sirari wilayani Tarime, naibu kamishna wa idara ya uhamiaji katika kituo hicho Gasper urio, amesema baada ya zoezi la mahojino kukamilika, serikali imeamua kuchukua hatua za kuwasafirisha wahamiaji hao hadi katika kambi za wakimbizi za umoja wa mataifa mkoani Kigoma

Kwa upande wao baadhi ya wakimbizi hao ambao wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wamesema wamelazimika kukimbilia nchini Tanzania kutoka kambi hiyo nchini Kenya baada ya kuchanganywa na wakimbizi kutoka nchini Somalia hatua ambayo imewapa hofu kubwa kuishi katika kambi hiyo.