Jumatatu , 1st Aug , 2022

Wadau wa Mahakama mkoani Kigoma wameazimia kwa pamoja kuanza kutekeleza adhabu mbadala kwa wafungwa ikiwemo kutoa likizo kwa lengo la kuwawezesha wafungwa kuandaa maisha nje ya kifungo na kuishi karibu na familia zao wakiendelea kufanya kazi za maendeleo.

Wafungwa

Adhabu mbadala kwa wafungwa ikiwemo kupewa likizo itahusisha wafungwa wenye vifungo chini ya miaka mitatu hatua itakayosaidia  kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani.

Mkurugenzi Msaidizi idara ya huduma za uangalizi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Charles Nsanze, amesema hatua hiyo itasaidia wafungwa kuzoeana na familia zao na kujiongezea kipato na kutoka vifungoni wakiwa tayari na mahusiano mazuri na familia.

Kwa upande wake Afisa Mhifadhi Wakimbizi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR mkoa wa Kigoma Rehema Msami, ambao wameratibu vikao vya kuwakutanisha wadau wa sheria mkoani Kigoma, wameomba pia wafungwa ambao ni wakimbizi kuwa sehemu ya mpango wa vifungo mbadala kulingana na sheria inavyoelekeza.