Jumatano , 11th Feb , 2015

Baadhi ya wafanyabiashara mjini Songea mkoani Ruvuma wamefunga maduka yao na kutokomea kusikojulikana kutokana nakesi inayomkabili mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania Johnson Minja.

PAMOJA na serikali kutoa tamko la kuwataka wafanyabiashara nchini kutofunga maduka na biashara wanazozifanya kwa sababu suala la kufunga maduka kuhusiana na kesi inayomkabili kiongozi wa wafanyabiashara lipo mahakamani, baadhi ya wafanyabiashara mjini Songea mkoani Ruvuma wamefunga maduka yao na kutokomea kusikojulikana.

Uchunguzi uliofanywa na EATV katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea umebaini kufungwa kwa maduka hayo huku wamiliki na wauzaji wa maduka hayo wakiwa hawajulikani walipo hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaohitaji huduma kutoka kwenye maduka hayo.

Wakizungumza baadhi ya wananchi akiwemo Ally Mpelasoka amesema taarifa za kufungwa kwa maduka zilianza kusambaa jana usiku kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao walisikika wakitoa angalizo kwa watakaofungua maduka yao kuanzia asubuhi ya Februari 11 mwaka huu wataonekana kuwa ni wasaliti wa uamuzi huo.

Wakati hali ikiendelea hivyo baadhi ya wafanyabiashara wadogo ambao hutegemea kuchukua bidhaa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa wamesema hawaelewi sababu ya kuwepo kwa agizo hilo kwa wafanyabiashara wote na wameziomba mamlaka zinazohusika kutatua mgogoro huo ambao ukiendelea utazidi kuwanyanyasa na kuwaathiri wananchi wakiwemo wakulima ambao wanahitaji kupata pembejeo za kilimo pamoja na vifaa vya ujenzi.

Juhudi za kuupata uongozi wa umoja wa wafanyabiashara wa mkoa wa Ruvuma kuzungumzia hali hiyo ya mgomo na hatima yake hazikuweza kufanikiwa baada ya kutokupatikana ofisini na kwenye simu zao za kiganjani.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkiririkiti alipozungumza kwa njia ya simu amesema wafanyabiashara ambao wengi wao ni watu wazima na wenye uelewa wanapaswa kutumia busara zaidi katika kutatua changamoto zinazojitokeza badala ya kufanya maamuzi ambayo yanaathiri makundi mengi wakiwemo wao wenyewe.