Alhamisi , 9th Jul , 2020

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma imekiri kuwaita na kuwahoji Wabunge wawili wastaafu wa Chama cha Mapinduzi, akiwemo Livingstone Lusinde 'Kibajaji' ambaye ilimhoji jana na Peter Serukamba ambaye bado inamshikiliwa kwa tuhuma za rushwa.

Kushoto ni Mbunge Mstaafu wa Mtera Livingstone Lusinde na kulia ni Mbunge Mstaafu wa Kigoma Kaskazini Peter Serukamba.

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 9, 2020 na Mkuu wa TAKUKURU Dodoma Sosthenes Kibwengo, wakati akizungumza na EATV&EA Radio Digital, huku akiwataka wanasiasa kuacha kujihusisha na michezo ya rushwa, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu. 

"Lusinde yeye tulipewa taarifa kwamba kuna Wajumbe wa CCM wamekusanywa nyumbani kwake wanahongwa, wanapewa ushawishi kwa ajili ya kufanya mambo fulani kuna 'scenario' mbili kwamba wamsaidie yeye maana ni mtia nia pia wamsaidie mama mwingine anaitwa Halima na yeye ni mtia nia, kwahiyo yote tunaendelea na uchunguzi" amesema Kibwengo.

"Serukamba na yeye ni ishu nyingine naye katika mambo hayo hayo kwamba tuna taarifa za tuhuma kwamba, anajihusisha na masuala ya rushwa masuala ya rushwa na yeye tuko naye Lusinde tumemhoji jana, atahojiwa tena kesho, lakini tunaye vilevile huyo Halima kwa ajili ya mahojiano" ameongeza.