
Vyama vya kiraia katika kesi ya uhaini ya rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimedai fidia ya mabilioni ya dola vikisema hii ni fidia kwa ghasia walizopitia mikononi mwa waasi katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa nchi hiyo.
Mashtaka dhidi ya Joseph Kabila ni pamoja na mauaji, ubakaji na mateso yanayohusishwa na madai yake ya kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo.
Katika mahakama ya kijeshi mjini Kinshasa, mawakili wa vyama vya kiraia wamesema wanatafuta karibu dola bilioni 25 za fidia na wamemtaja Kabila kama "raia wa Rwanda" wakidai ahukumiwe kwa kosa la ujasusi badala yake. Wakati huo huo, majimbo ya mashariki ya Kivu Kusini, Ituri na Kivu Kaskazini yanadai nyongeza ya dola bilioni 21 na kutwaliwa kwa mali ya benki ya rais huyo wa zamani.
Kufuatia miaka miwili ya uhamisho wa kujitegemea nchini Afrika Kusini, Kabila alirejea Goma mwezi Mei baada ya mji huo kutekwa na kundi linaloungwa mkono na Rwanda, lakini anahukumiwa bila kuwepo. Amekanusha kuwa nyuma ya waasi au mmoja wa waanzilishi wa Muungano wa Mto Kongo (AFC), kundi kubwa la waasi ambalo linajumuisha M23 na wanamgambo wengine, ameikataa kesi hiyo akiitaja kuwa ya kiholela"na kusema mahakama zinatumika kama "chombo cha ukandamizaji".
Wakati marais wa zamani wanahudumu kama maseneta maisha na kufurahia kinga ya maisha, Kabila alinyang'anywa ulinzi huu mwezi Mei ili kuruhusu mashtaka yake. Mwanasheria mkuu wa jeshi hilo anatarajiwa kuwasilisha hoja zake za mwisho kuhusu kesi hiyo siku ya leo Ijumaa